Serikali inaendelea kujenga uchumi imara - Mwijage
Hayo ameyasema wakati akihitimisha Maonesho ya (SIDO) Kitaifa yaliyofanyika katika Viwanja vya Nyakabindi Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu, yakiwa na Kauli Mbiu: “PAMOJA TUJENGE VIWANDA KUFIKIA UCHUMI WA KATI”
Mhe. Mwijage amezitaja baadhi ya sifa za uchumi wa Kitaifa (Jumuishi) kuwa ni pamoja na Kipato cha wastani kwa Mtanzania kufikia dola 3000 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025, Watanzania kuwa na maisha mazuri, watu kuwa na elimu na wepewi kwa kujifunza, pamoja na kuwa na uchumi imara ulio shindani.
“Tunataka mwaka 2025 tuwe na uchumi imara na shindani lakini tuendelee kudumisha amani na msihikamano; njia rahisi ya kufikia mahali mbapo kipato cha wastani cha Mtanzania kuwa dola 3000 kwa mwaka ni kupitia uchumi wa viwanda na uchumi wa viwanda ni zaidi ya viwanda, uchumi wa viwanda unaanzia shambani hadi sokoni” alisema.
Katika hatua nyingine alitoa wito kwa Watanzania kulinda viwanda vya ndani hapa nchini kwa kununua bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Mhe. Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema Mapinduzi ya viwanda yanatokana na Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO), hivyo ni vema wizara ya viwanda ,biashara na uwekezaji ikaliwezesha shirika la kuhudumia viwanda vidogo ili kutekeleza azma ya Tanzania ya viwanda.
Akizungumzia maonesho ya Viwanda vidogo Mkurugenzi Mkuu wa SIDO Prof. Silvester Mpanduji, amesema jumla ya wajasiriamali 515 kutoka mikoa 23 nchini na nchi jirani za Uganda na Burundi, wameshiriki manesho haya na kupata fursa ya kuonesha bidhaa wanazozalisha na kubadilisha uzoefu katika masuala mbalimbali.
Aidha, amesema kupitia maonesho hayo mashine za kuongeza thamani katika mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu zenye thamani ya zaidi ya shilingi 800 zimenunuliwa na nyingine kuwekewa ahadi ya kununuliwa.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa UNDP anayeshughulikia miradi Amoni Manyama ameahidi kuwa Shirika hilo liko tayari kushirikiana na Serikali hapa nchini katika Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda kwa kutoa msaada wa kifedha na utaalam wa kuchambua miradi ya viwanda katika Mkoa wa Simiyu na mikoa mingine pia.
Maonesho ya Viwanda Vidogo SIDO Kitaifa yaliyofanyika kwa muda wa siku sita katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu yalifunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Oktoba 23, 2018, pamoja na wajasirimali 515 kushiriki takribani taasisi za Umma na Binafsi 24 zimeshiriki maonesho haya.
Serikali inaendelea kujenga uchumi imara - Mwijage
Reviewed by Zero Degree
on
10/29/2018 07:35:00 AM
Rating: