Loading...

TTCL kupunguza wafanyakazi zaidi ya 500


SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) litapunguza wafanyakazi 555 kutoka 1,500 waliopo ili kubaki na 945 kwa lengo la kuboresha muundo mpya wa shirika hilo.

Akielezea mkakati wa biashara wa shirika hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TTCL, Omari Nundu amesema, wengi wa hao watakaopunguzwa ni wale wasioendana na kasi ya teknolojia ya mawasiliano na hawawezi kubadilika.

Nundu alisema kupunguzwa huko kunaenda sambamba na uboreshaji wa huduma za shirika hilo ambalo pamoja na mikakati mingine, limepanga kupanua soko la watumiaji wa mtandao wake kwa kuongeza wateja ambao ni wachache ukilinganisha mitandao ya mawasiliano mingine.

Alisema shirika pia linaboresha huduma zake, ikiwamo kuanzisha huduma ya T-Pesa ambayo inashughulika na miamala ya fedha, lengo ni kupambana katika soko hilo na malengo ni kuhakikisha pia serikali inatumia muamala huo katika kupokea na kutoa fedha za huduma kwa umma.

Alisema shirika hilo ni namba moja katika uuzaji wa huduma za jumla za mawasiliano kwa kampuni nyingine za mawasiliano, sasa linataka kuingia kwenye kukuza huduma za mawasiliano na kuwafikia wananchi vijijini ambao hawajafikiwa na kampuni nyingine.

Nundu alisema ili kufika katika maeneo hayo, shirika hilo limeshaingia mkataba na Tigo ili kutumia minara yao, kitendo ambacho kimesaidia kuwafikia wananchi wengi katika maeneo mbalimbali.

Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba amesema, katika mkakati wake wa miaka mitano, wamejipanga upya kuboresha huduma zake za kujinadi kwa kuajiri wafanyakazi wengine wa kitengo hicho muhimu katika mawasiliano.

Amesema ukiangalia katika umiliki wa soko la huduma za mawasiliano ya rejareja wapo chini, lakini katika utoaji huduma za mawasiliano za jumla inaongoza kwa asilimia 85, ikiongoza kwani kampuni nyingine zinaitegemea.

Alisema kwa sasa shirika hilo lina sheria ya asilimia 1.3 ya soko la mawasiliano ambayo ni ndogo ukilinganisha na kampuni nyingine za mawasiliano kama Vodacom yenye asilimia 32, Tigo (28), na Airtel (26).

Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), Dk Raphael Chegeni alilitaka kubadilika na kuitendea haki kauli ya Rais John Magufuli ya “Rudini Nyumbani Kumenoga” kwa kuweka mikakati ya kujitangaza.

Amesema TTCL haijajipanua kibiashara na hivyo kushindana kwenye soko la mawasiliano na wenzao, hivyo wanatakiwa kuweka mikakati, malengo, kuongeza ufanisi na utendaji ili kuitendea haki kauli ya Rais ya rudini nyumbani kumenoga.

Alisema inatakiwa kuboresha huduma kwa kuweka mkakati wa kibiashara wenye ushindani na mashirika au taasisi nyingine zinazotoa huduma ya mawasiliano nchini.

Pia aliitaka kupunguza gharama za uendeshaji kutovuka asilimia 60 kama sheria inavyotaka, lakini pia inatakiwa kupunguza watumishi ambao hawawezi kwenda na mabadiliko na kasi ya mageuzi ya teknolojia ya sasa.

Dk Chegeni pia aliagiza ndani ya siku 14 kupeleka maelezo kupitia kwa Msajili wa Hazina (TR) wakieleza uhusiano wake na Airtel kama kweli inamilikiwa na shirika hilo kwa asilimia 100 au vinginevyo kwani kumekuwa na utata.

Source: Habari Leo
TTCL kupunguza wafanyakazi zaidi ya 500 TTCL kupunguza wafanyakazi zaidi ya 500 Reviewed by Zero Degree on 10/31/2018 12:05:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.