Jeshi la polisi Shinyanga laua majambazi wawili
Jeshi la Polisi linasema tukio hilo lilitokea wakati watuhumiwa hao wakiwakimbia askari walipokuwa wakijibizana kwa risasi na wenzao, ambao walikwenda kukamatwa katika eneo ambalo hujificha kwenye vichaka la Buhaghija mjini hapo.
Tukio hilo limetokea jana usiku, wakati majambazi hao wakiwapeleka askari polisi kuwaonyesha mahali ambapo wamejificha wenzao kwenye vichaka hivyo, kama eneo lao la kukutana kupanga njama kabla ya kwenda kufanya uhalifu.
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Simon Haule, aliwataja watuhumiwa waliouawa kuwa ni Godfrey Ntabazi (29), mkazi wa Mahina jijini Mwanza, na Ramadhani Masoud (33), mkazi wa Ngokolo mjini Shinyanga, na kwamba miili yao imehifadhiwa kwenye hospitali ya mkoa huo.
“Majambazi hawa wawili awali tulikuwa tumewakamata na baada ya kuwahoji tukawaamuru watupeleke kwa wenzao mahali ambapo huwa wanakutana, na baada ya kufika eneo la tukio risasi zikaanza kurindima kutoka kwa wenzao, na wao wakaanza kutukimbia ndipo tukawapiga risasi,” alisema Haule.
“Wakati tukiwakimbiza kwenda kupatiwa matibabu katika hospitali ya rufani ya mkoani hapa, walifariki dunia wakiwa njiani, huku wenzao wakifanikiwa kutoroka na tunaendelea kuwasaka ili tuwatie nguvuni na kuchukuliwa hatua kali za kisheria,” aliongeza.
Alisema katika eneo la tukio zilikamatwa bunduki mbili pamoja na risasi nne, ambazo zilikuwa zikitumiwa kufanyia uhalifu katika maeneo mbalimbali ya mkoani Shinyanga, Geita na Tabora, na kubainisha kuwa majambazi hao ni sugu na walishafungwa jela mara nyingi.
Aidha, alisema jeshi hilo pia lilifanya upekuzi nyumbani kwa watuhumiwa hao wa ujambazi, ambapo kwa Godfrey Ntabazi walikuta akiwa na chupa za pombe mbili aina ya K-Vant, dawa ya kuwekea mbwa ili kuwafubaza na nyumbani kwa Ramadhani Masoud walikamata TV nne, deki tano, sabufa tatu na baiskeli moja.
Jeshi la polisi Shinyanga laua majambazi wawili
Reviewed by Zero Degree
on
2/07/2019 03:20:00 PM
Rating: