Loading...

Mshahara wa Tundu Lissu waingia mashakani



Safari na mahojiano ya Mbunge wa Singida Mashariki nchini Tanzania Tundu Tundu Lissu zinaendelea kuzua mjadala nchini humo na sasa limetolewa pendekezo kuwa mshahara wake Bungeni usitishwe.

Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana nje ya makazi yake mjini Dodoma Septemba 17, na toka wakati huo yupo nje ya Tanzania ambapo amekuwa akipokea matibabu.

Awali alianzia jijini Nairobi Kenya, na mwaka mmoja uliopita kuhamishiwa Ubelgiji.

Hata hivyo, katika majuma ya hivi karibuni Lissu ametoka Ubelgiji na kuzuru nchini Uingereza na kufanya mahojiano na runinga ya BBC, Kisha akazuru Ujerumani na kufanya mahojiano na runinga ya DW. Kwa sasa yupo nchini Marekani na ameshafanya Mahojiano na runinga ya VoA.

Kote huko, Lissu ambaye ni mbunge kupitia chama cha upinzani cha Chadema ameendelea kusisitiza kuwa serikali ya rais John Magufuli ilikuwa na mkono kwenye shambulio dhidi yake. Pia amelishambulia Bunge chini Spika Job Ndugai kwa 'kumtelekeza' na kushindwa kulipia matibabu yake nje ya nchi.

Kauli hizo zimekuwa zikichochea mjadala ndani ya Tanzania na leo hii suala hilo limejadiliwa Bungeni.

Mbunge wa Geita (CCM), Joseph Kasheku 'Musukuma' amehoji kupitia Mwongozo wa Spika ni lini Bunge litasitisha mshahara wa Lissu aliyedai kuwa amepona na sasa anaitukana Serikali na Bunge.

Spika Ndugai amesema atafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kushughulikia hoja ya kusitisha mshahara wa Tundu Lissu.

Musukuma ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 7, 2019 bungeni jijini Dodoma baada ya kuomba mwongozo wa Spika.

"Lissu anazurura duniani huku anasemekana anaumwa, ni lini Bunge litasitisha mshahara wake kwa sababu ameshapona na ameendelea kuzunguka huko na huko akitukana Bunge na Serikali," amehoji Musukuma.

Akijibu mwongozo huo, Spika Ndugai amesema hoja ya Msukuma ina mashiko na suala hilo linahitaji kuangaliwa kwa upekee.

"Jimboni hayupo, bungeni hayupo, nchini hayupo, hospitali hayupo na mimi sina taarifa yake yoyote wala ya daktari, na wala haangaiki kunijuza wapi alipo. Hoja yako ina msingi iko haja ya kusimamisha mishahara wake. Na nikuhakikishie kuwa yale yaliyo ndani ya uwezo wangu nitayafanya," amesema Ndugai.

Tundu Lissu: 'Chama kikisema mimi nafaa, niko tayari kuwa rais Tanzania'

Wiki moja iliyopita, baada ya Lissu kurejelea hoja yake kuwa Bunge halijamlipia hata mara moja katika matibabu yake nje ya nchi Spika Ndugai alikanusha madai hayo kuwa ni ya uongo.

Ndugai alidai dai kuwa hadi mwishoni mwa Desemba 2018, Lissu alikuwa amelipwa Sh207.8 milioni pamoja na Sh43 milioni zilizotolewa kama mchango wa matibabu yake na wabunge wenziwe na kufanya jumla kuu ya fedha alizolipwa kuw Sh250milioni.

Lissu amekiri kulipwa Sh43 milioni zilizotolewa na wabunge wenzake kama mchango wao na kwamba kiasi kingine alicholipwa kinachofanya jumla ya fedha hizo kufikia Sh250 ni mishahara na stahiki zake, lakini siyo gharama za matibabu.


Chanzo: BBC
Mshahara wa Tundu Lissu waingia mashakani Mshahara wa Tundu Lissu waingia mashakani Reviewed by Zero Degree on 2/07/2019 06:50:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.