Loading...

Watuhumiwa kesi bomba la mafuta waachiwa huru


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewafutia mashtaka na kuwaachia huru, washtakiwa watano waliokuwa wanakabiliwa na tuhuma za kujiunganishia isivyo halali bomba la mafuta, mali ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Uamuzi huo ulitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, wakati kesi hiyo ilipopangwa kwa ajili ya kutajwa.

Awali upande wa Jamhuri ulidai kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) anaomba kuwaondolewa washtakiwa mashtaka yao kwa sababu hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Simon Wankyo, alidai kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa lakini DPP hana nia ya kuendelea na kesi dhidi ya mshtakiwa hao.

Washtakiwa hao wamefutiwa mashtaka hayo chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Kwa mujibu wa taarifa ya Gazeti la Nipashe, hakimu Simba alisema kupitia kifungu hicho mahakama imewafutia mashtaka washtakiwa hao watano na imewaachia huru.

Washtakiwa waliofutiwa kesi ni Audai Ismail (43) ambaye ni mkazi wa Kibaha, Chibony Emmanuel, Roman Abdon, Amina Shaban na Zubery Ally.

Hakimu Simba alisema kupitia kifungu hicho namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), DPP anao uwezo wa kuwakamata na kuwafungulia mashtaka, washtakiwa hao.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa hao wanadaiwa kati ya mwaka 2015 hadi Januari 8, 2018 katika eneo la Tungi Muungano wilayani Kigamboni, walijiunganishia bomba la mafuta ya dizeli lenye upana wa inchi moja kutoka katika bomba lenye upana wa inchi 24 bila kuwa na kibali.

Katika shtaka la pili washtakiwa walidaiwa kuharibu miundombinu na kwamba siku hiyo ya tukio, walitoboa bomba la hilo ambalo lilikuwa likitumika kusafirisha mafuta mali ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Katika shtaka la tatu, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuharibu bomba la mafuta mazito (crude oil) lenye upana wa inchi 28, ambalo lilikuwa likitumika kusafirisha mafuta ghafi, mali ya TPA.
Watuhumiwa kesi bomba la mafuta waachiwa huru Watuhumiwa kesi bomba la mafuta waachiwa huru Reviewed by Zero Degree on 9/24/2019 07:50:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.