Loading...

Dkt. Mpango ameweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Daraja la Mto Hurui

Makamu wa Rais Dk Philip Mpango akiweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Daraja la Mto Hurui lililopo katika Kijiji cha Hurui Wilaya ya Kondoa akiwa ziarani mkoani Dodoma leo Agosti 21

Makamu wa Rais Dk Philip Mpango ameiagiza Wakala wa Barabara Mijini na Vijiji (TARURA) kufanya ukarabati wa Barabara ya Ntundwa – Hurui ya Wilayani Kondoa ili kuwarahisishisa wananchi shughuli za kiuchumi ikiwemo usafirishaji mazao.

Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo leo Agosti 21 mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la mto Hurui lililopo kata ya Kikore Wilaya ya Kondoa akiwa ziarani mkoani Dodoma.

Amewahimiza wananchi wa kata ya Kikore na watumiaji wa daraja hilo kutunza miundombinu iliyojengwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadaye.

Dk Mpango amewaagiza kupanda miti maeneo yote pembezoni mwa mto hurui ili kuokoa daraja hilo lisiharibike kutokana na mmomonyoko wa udongo.

Makamu wa Rais amewapongeza wananchi hao kwa kupata mradi wa daraja uliowaondolea changamoto waliyopata ya kukosa daraja tangu mwaka 2019 lilipoharibiwa na maji daraja la awali. Amewahakikishia wananchi hao serikali itaendelea kuwafikishia wananchi huduma muhimu ikiwemo miundombinu.

Makamu wa Rais akiwa katika kata ya Kikore ameagiza kukamilishwa kwa mradi wa maji unaotekelezwa katika kata hiyo ifikapo Oktoba 30 mwaka huu.

Aidha ameiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini kushughulikia changamoto iliyotolewa na wananchi wa Kijiji cha Hurui kuhusu ardhi ya Kijiji inayodaiwa kuuzwa kwa mwekezaji bila kufuata utaratibu.

Ujenzi wa Daraja la Hurui umegharimu shilingi bilioni 1.6 na linatarajiwa kuwa kiungo muhimu na kufungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa kurejesha mawasiliano kati ya Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma na Wilaya ya Babati mkoani Manyara.


Daraja hilo lenye urefu wa Mita 30 limejengwa kwenye barabara ya Ntundwa – Mkunduru -Hurui yenye urefu wa kilometa 46.4.

Mradi huo umehusisha uboreshaji wa kilometa 8 za barabara kwa kiwango cha changarawe na umegharamiwa na Serikali kupitia tozo ya mafuta ya shilingi 100.
Dkt. Mpango ameweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Daraja la Mto Hurui Dkt. Mpango ameweka Jiwe la  Msingi Ujenzi wa Daraja la Mto Hurui Reviewed by Zero Degree on 8/21/2024 04:56:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.