Loading...

Kocha Boniface Mkwasa aponzwa na misimamo yake.


Siku moja baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumpa jukumu la kuinoa timu ya Taifa, kocha mkuu wa Mtibwa Sugar, Salum Mayanga, wadau wa soka wamedai kuwa moja ya sababu zilizomwondoa Charles Mkwasa ni kutokana na misimamo yake.

Baadhi ya wadau hao walidai kuwa misimamo na namna Mkwasa anavyosimamia mambo yake imekuwa moja ya sababu zilizomponza katika nafasi hiyo ya kuinoa Stars aliyodumu nayo tangu Julai 2015.

Kwa upande wake, mrithi wake, Mayanga, alisema jukumu hilo jipya kwake lina changamoto zake na atalizungumzia zaidi atakapokabidhiwa rasmi barua ya uteuzi wake.

Mayanga alisema atatoa taarifa kamili baada ya kukamilika kwa mazungumzo na wakuu wa TFF.

“Bado hata sijapewa barua rasmi kwa hiyo ni vigumu kusema nitafanya nini, lakini kimsingi ni jukumu lenye changamoto na linalopaswa kuangalia jinsi gani ya kufanya,” alisema Mayanga akizungumza na kituo kimoja cha redio jijini Dar es Salaam jana.

Kutwa nzima ya jana zilifanyika juhudi za kuzungumza na Mayanga na awali alikubali na kusema atafutwe, lakini alipopigiwa simu iliita na baadaye kutopatikana hewani.

Licha ya kwamba si mgeni na Taifa Stars kwa kuwa aliwahi kuwa kocha msaidizi wakati wa Kocha Martin Nooij mwaka 2014/15, pia aliwahi kuwa kocha mkuu wa timu ya Stars Maboresho (Young Taifa Stars) ambayo mapema 2014 iliweka kambi ya miezi mitatu wilayani Rungwe Mkoa wa Mbeya. Jukumu linalomkabili ni kuiandaa timu ya Taifa kwa ajili ya michuano ya kufuzu fainali za mataifa mwaka 2019.

Kabla ya kukabidhiwa jukumu hilo Mayanga aliwahi kuzinoa Mtibwa na Prisons kwa nyakati tofauti na mwaka jana, alisaini mkataba wa miaka miwili wa kuifundisha Mtibwa Sugar.

Wamtetea Mkwasa


Akizungumzia hatua ya TFF kuachana na Mkwasa, mshambuliaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Abeid Mziba alisema ameondolewa kwenye wadhifa wake kwa sababu ya siasa na fitna zinazoendekezwa na viongozi wa soka nchini.

“Mayanga na Mkwasa nani yuko juu? Wameangalia vigezo gani hasa?” Alihoji Mziba.

“Mkwasa ni mara 10 ya Mayanga, hata katika klabu walizofundisha, amefanya vizuri kuliko Mayanga na ana uzoefu wa kutosha.

“Mkwasa ni mtu mwenye misimamo yake, inawezekana wameamua kumchukua Mayanga kwa kuwa anaendana na wanayoyataka. Ndiyo maana soka letu halipigi hatua,” alisema Mziba

Katibu Mkuu wa Prisons, Oswald Morris alisema Mayanga ni miongoni mwa makocha bora wazawa waliopo nchini na kumtahadharisha kuwa makini wakati wa utekelezaji wa majukumu yake.

“Ni kocha aliyefanikiwa na ninafikiri TFF imeangalia uwezo wake, lakini anatakiwa kuangalia na timu za mikoani anapofanya uteuzi wa timu ya Taifa.

“Ajitofautishe na makocha waliopita waliokuwa wanaita wachezaji waliopo Dar es Salaam, anatakiwa kuangalia na timu za mikoani ambazo zina wachezaji wazuri wanaoweza kuisaidia nchi.

“Huu haukuwa wakati mwafaka kwa Mkwasa kuondoka Stars, angalau wangempa miaka miwili zaidi ya kuinoa Stars,” alisema kiungo wa zamani wa Yanga na Stars, Yusufu Macho.

Macho alisema Mayanga asingepewa jukumu la kocha mkuu badala yake angekuwa msaidizi wa Mkwasa ambaye amemtaja kama kocha kwake anaona alistahili kuendelea kuinoa Stars. Mshambuliaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ally Yusuph ‘Tigana’ alisema alipaswa kupewa muda zaidi.

“Mkwasa aliwahi kuwa kocha wangu nikiwa Yanga kwenye miaka ya 2000 na 2001 kuondoa mambo mambo yake binafsi, bado ni kocha mzuri.

“Kiwango chake siwezi kukulinganisha na Mayanga kwa sababu ameingia kwenye soka nikiwa nimestaafu, lakini Mkwassa yuko vizuri na kwangu naona alistahili kuwa na timu ya taifa kwa muda mrefu zaidi,” alisema Tigana.

Kipa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Kitwana Manara alisema hajaona sababu ya kumwondoa Mkwasa.

“Sijui kilichomuondoa, pia anayekuja siwezi kueleza atakuwa na kipya gani, lakini kinachotakiwa ni wote kushirikiana na Mayanga apewe muda wa kufanya kazi yake, kimsingi awe huru na wachezaji wa Taifa Stars wawe na moyo wa kujituma,” alisema Kitwana.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella alisema soka ndivyo lilivyo na makocha wanaajiriwa ili wafukuzwe, hivyo hashangazwi kwa Mkwasa kuondoka.

“Huwezi kujua huyo anayemrithi huenda akawa na Mungu, akafanya vizuri zaidi au akavurunda zaidi, soka ni kama mchezo wa kamari, cha msingi tumpe muda,” alisema Mogella.

Kiungo wa Azam na Taifa Stars, Himid Mao ambaye alifanya kazi na Mkwasa katika muda wote aliokuwa na timu, alisema watamkumbuka Mkwasa kwa kuwa alijua kuishi na wachezaji na kumtakia kila la kheri Mayanga.

Mkwasa aomba radhi


Kwa upande wake, Mkwasa alisema anaomba radhi kwa kutofikia matarajio kwa majukumu aliyokabidhiwa na kusema ndivyo soka ilivyo.

Alisema anahitaji kupumzika hadi mkataba wake utakapomalizika na hata kama kuna timu inamuhitaji, isubiri hadi mkataba wake utakapomalizika.

“Tumeafikiana na uongozi wa TFF, watanilipa fedha kati ya mwezi wa kwanza na wa pili, lakini yaliyopita si ndwele tugange yajayo, Watanzania waendelee kuisapoti timu yao,” alisema Mkwasa Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Alfred Lucas alitaja vigezo vilivyozingatiwa kumpata Mayanga kuwa ni uzoefu, elimu na mafanikio ya kocha huyo katika klabu.




Source: Mwananchi
ZeroDegree.
Kocha Boniface Mkwasa aponzwa na misimamo yake. Kocha Boniface Mkwasa aponzwa na misimamo yake. Reviewed by Zero Degree on 1/04/2017 12:32:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.