Loading...

Askari watuhumiwa kuua mahabusu mkoani Simiyu

MAHABUSU Masasi Makelebende (32), mkazi wa kitongoji cha Badabada mjini Maswa mkoani Simiyu, amekufa katika mazingira yanayoelezwa kuwa ni ya utatanishi katika Gereza la Mahabusu la Wilaya ya Maswa.

Hata hivyo, uongozi wa gereza hilo ulisema kuwa mahabusu huyo amekufa kwa maradhi, taarifa ambazo zinakinzana na zile zinazotolewa na mahabusu wengine waliopo ndani ya gereza hilo wanaodai kuwa aliuawa kwa kupigwa na askari.

Taarifa zilizopatikana kutoka kwa ndugu na jamaa wa marehemu zinaeleza kuwa kifo hicho kimesababishwa na kipigo kutoka kwa baadhi ya askari Magereza wa gereza hilo (majina yanahifadhiwa).

Wakizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama ya Wilaya ya Maswa jana kwa masharti ya kutoandikwa majina yao gazeti, baadhi ya mahabusu walisema kuwa mahabusu huyo alifikwa na umauti baada ya kupigwa alipokutwa akiwa na sigara aina ya tumbaku, Februari 10, mwaka huu.

“Siku hiyo kulikuwa na oparesheni ndani ya gereza ya kusaka wafungwa na mahabusu wanaotumia sigara na msako huo ulianza selo hadi selo na katika msako huo marehemu pamoja na mahabusu mwingine walikutwa wakiwa na sigara ya tumbaku iliyosokotwa kwa kipande cha gazeti.

“Baadaye ilitolewa amri kuwaamuru askari Magereza waanze kuwapiga ili waeleze ni askari gani wanaowasaidia kuingia na tumbaku ndani ya gereza lakini hawakuweza kusema ndipo walipoendelea kupigwa hadi wote wakapoteza fahamu,” alisema mmoja wa mahabusu.

Mahabusu hao waliendelea kueleza kuwa baada ya mahabusu hao kupoteza fahamu alifika daktari wa gereza ili kuwafanyia vipimo ndipo alipobaini kuwa mmoja alikuwa amefariki dunia huku mwingine akiwa mahututi.

Walisema baadaye mwili wa marehemu na mahabusu mahututi waliingizwa katika gari dogo na kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa.

Walisema hatua hiyo iliwafanya mahabusu na wafungwa wengine kugoma kula kwa muda wa siku mbili wakishinikiza askari wote waliohusika na kifo cha mwenzao wachukuliwe hatua za kisheria, hadi pale Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Seif Shelakaghe alipofika na kuzungumza na wafungwa na mahabusu hao bila kuwepo askari.

Ndugu wa marehemu Emanuel Mlyanzenze alisema kuwa Februari 1,1 mwaka huu walipata taarifa kuwa ndugu yao aliyekuwa mahabusu katika gereza la Maswa ambaye alikuwa akikabiliwa na kesi ya mauaji amefariki dunia.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Shelakaghe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya hiyo amekiri kutokea kwa tukio hilo na kusisitiza kuwa askari wote wanaotuhumiwa wameondolewa katika gereza la Maswa ili kupisha uchunguzi.

Source: Habari Leo
Askari watuhumiwa kuua mahabusu mkoani Simiyu Askari watuhumiwa kuua mahabusu mkoani Simiyu Reviewed by Zero Degree on 2/26/2017 11:32:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.