Loading...

Jinsi Siasa inavyoyumbisha wasanii nchini

Wasanii wa muziki wa kizazi kipya na wale wa Bongo Movie, wameonywa kwamba kujiingiza kwao kwenye siasa kunaweza kuwa chanzo cha kudidimiza vipaji vyao na kutoweka katika ulimwengu wa sanaa.

Gazeti la mwananchi lilifanya uchunguzi kuhusiana na taarifa za siasa kuwamaliza wasanii ambapo wadau mbalimbali walitoa maoni yao, akiwamo waziri mwenye dhamana na wasanii, Nape Nnauye na mwanamuziki mkongwe nchini, John Kitime

Taarifa zilizozagaa ni kwamba wasanii wengi waliovuma miaka ya nyuma, kwa sasa wametoweka baada ya kushiriki kampeni za kisiasa za Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Uchaguzi huo uliokuwa na joto kali la kisiasa kutokana na nguvu waliyokuwa nayo wagombea wawili, John Magufuli wa CCM na Edward Lowassa aliyesimamishwa na Ukawa kupitia Chadema, ulionekana kuyumbisha wasanii wengi.

Mfano, katika uchaguzi huo wasanii wengi walishiriki kupigia kampeni wagombea urais, kuna waliokuwa CCM na wengine Ukawa. Na baada ya hapo wengi wametoweka katika ulimwengu wa sanaa.

Kitime ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya sanaa, alisema kutokana na uchanga wa demokrasia, msanii anaposhabikia chama fulani wakati mashabiki wake wana mrengo tofauti unajengeka uadui na kupoteza mashabiki.

“Hasara zilizopo kwa msanii ni kupoteza mashabiki kwa kuwa demokrasia yetu bado haijakua, lakini pia anaweza kupoteza mwelekeo ikiwa chama alichokishabikia hakitashika dola huenda ikamwathiri pia kwa kukosa fursa nyingi na kuwekwa pembeni katika kila shughuli,” alisema Kitime.

Alisema hata hivyo kizazi cha sasa kimekuwa huru kujipambanua ukilinganisha na enzi zao.

Kitime aliweka wazi kwamba huenda hiyo ndiyo sababu ya wanamuziki wakongwe kushindwa kujihusisha na masuala ya kisiasa kwa sasa.

Alisema licha ya wasanii wengi kujipambanua pia walio wengi wanaangalia zaidi faida zitokanazo na masuala ya kampeni za kisiasa pasipo kung’amua hasara zake baadaye.

Kitime alisema miaka ya 1970 hadi 1980 wasanii walio wengi ilikuwa lazima wawe na kadi za chama cha TANU na ilikuwa kama kitambulisho cha uraia.

Kadi ya chama ilitumika msanii alipotaka nafasi ya kusafiri nje ya nchi au hata kuitumia kufungua akaunti benki, kibali cha shoo pia ilikuwa ni kadi ya chama.

“Kwetu ilikuwa ni kama kitambulisho, kwa maana hakukuwa na chaguo la ziada, ilitulazimu kuwa huko na tulitumbuiza kwa kuwa wananchi wote walikuwa katika chama kimoja. Hakuna mtu ambaye alikuwa anazifikiria hasara za upande wa pili, tulishiriki katika masuala ya Mwenge wa Uhuru, sherehe mbalimbali za kitaifa yaani kadi ilituwezesha hivi vyote,” alisema Kitime.

Kitime alisema wasiwasi wake unakuja kwa kile alichokiita demokrasia na siasa za vyama vingi ambapo alisema vyama vinawatumia wasanii kujinufaisha.

Uchaguzi wa mwaka 2015 wapo waigizaji walioamua kudhihirisha kuwa wanashabikia chama fulani kwa mfano Jackline Wolper, Aunty Ezekiel, Shamsa Ford walitangaza kuwa wanashabikia Chadema wakati wasanii Batuli, Wastara Juma, Jenifer Kyaka ‘Odama’ Wema Sepetu, Steve Nyerere, JB na wengine waliishabikia CCM.

Hata hivyo, baadaye Wolper na wenzake waliokuwa Chadema kipindi hicho hicho cha uchaguzi walitangaza kujiunga CCM wakidai walipotea njia.

Juni 2015 Mrembo wa Taji la Miss Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu alitangaza rasmi nia ya kuwania ubunge wa viti maalum mkoa wa Singida kwa tiketi ya CCM.

Wema aliyedai kuwa yeye ni mwana CCM tangu mwaka 2010, hivi karibuni alitangaza kuhamia Chadema Februari 24 mwaka huu. Tangu aanze harakati hizo za siasa Wema hajatoa filamu mpya.

Hata hivyo, Meneja wa Yamoto Band, Said Fella alisema ushiriki wa kundi hilo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 si sababu ya kuporomoka kisanii.

“Kwetu siasa ina nafasi yake na muziki hali kadhalika, ndiyo maana waliposhiriki kwenye kampeni meneja wao alikuwa Chambuso, sikusimama mimi na vivyo hivyo kwa sasa bado wapo na wanafanya muziki kama kawaida,” alisema Fella.

Mwimbaji wa muziki wa Zouk nchini, Mwasiti Almas alisema alishiriki katika siasa kwa vipindi viwili tofauti, lakini alijitahidi kuwa mtumbuizaji zaidi kuliko kujipambanua anashabikia chama gani na hicho ndicho walio wengi wanakikosea.

“Unapokuwa msanii fanya sanaa na achana na siasa, haya mambo mawili hayachangamani kwa kuwa mashabiki wako ni wa pande zote, ukijitangaza unashabikia wapi umeumia,” alisema Mwasiti.

Kuhusiana na hilo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alisema hoja kwamba wasanii kuingia kwenye siasa kunawapoteza inahitaji upembuzi wa kina.

Alisema kuna mambo mengi yanaweza kuchangia, lakini alitoa mfano wa soko la filamu kwa kuwataka wazalishaji kueleza namna soko lilivyoshuka.

Nape alisema badala ya kwenda na kauli za jumla ni vema kuwa na takwimu ambazo zinaelezea awali waliuza nakala ngapi kwa filamu moja na sasa wanauza ngapi.

Hata hivyo, alisema amekuwa akifuatilia soko la filamu za ndani ya nchi kwa ukaribu tangu amekuwa waziri wa wizara hiyo, hivyo kuwabana zaidi wezi wa kazi zao kulifanya soko hilo kuyumba.

“Mmeshuhudia nafanya oparesheni mitaani, najua kilichoshusha kazi za wasanii wa ndani ni piracy ‘wizi wa kazi za wasanii’, kazi za sanaa zilizopo mtaani ambazo hazijalipiwa kodi ndizo zimeshusha mauzo ya kazi za wasanii, hili ndilo suala la msingi, haya mengine ni hisia za watu ambao mimi nisingependa nilizungumzie,” alisema Nape.

Rapa msomi kutoka Kundi la Weusi, Nickson Simon maarufu ‘Nikki wa Pili’ alisema wanasiasa ndiyo ambao huwatumia wasanii na siyo siasa.

Alisema kwa sasa wanasiasa kuwatumia wasanii ni jitihada zilizofilisika kwa maana siasa inatakiwa kubebwa na mambo ya kijamii, mwanasiasa anatakiwa kuongea kuhusiana na mambo yanayoifika jamii na namna ya kukabiliana nayo.

“Mwanasiasa unapoamua kuwatumia wasanii maana yake unataka kutumia propaganda, hizo ni siasa zisizo bora kwani unaanza kutegemea wasanii badala ya fikra, uchambuzi, dhana,” alisema.

Alisema hiyo huleta migongano kwa maana wanasiasa haohao baadaye huanza kuhoji maadili ya kazi za wasanii, lakini kipindi cha uchaguzi wapo ambao walikuwa wanalipwa waimbe nyimbo ambazo hazifai kwa jamii.

“Mwanasiasa anapomtumia msanii hajali maadili yake anachoangalia ni idadi ya wafuasi wa msanii. Ukubwa wa msanii ndiyo mtaji kwa mwanasiasa huyo wakati wa kampeni,” alisema.

Nikki wa Pili alisema hiyo ndiyo sababu hata filamu zao hukosa maadili.

Source: Mwananchi
Jinsi Siasa inavyoyumbisha wasanii nchini Jinsi Siasa inavyoyumbisha wasanii nchini Reviewed by Zero Degree on 2/27/2017 12:20:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.