Loading...

Wasichana waliovaa nguo za kubana wazuiliwa uwanja wa ndege Marekani


Ndege ya Shirika la United Airlines nchini Marekani
Shirika la ndege la United Airlines nchini Marekani limeshutumiwa sana baada ya kudaiwa kuwazuiwa wasichana wawili waliokuwa wamevalia suruali ndefu za kubana kuabiri ndege hiyo.

Kisa hicho kilitokea kwenye safari ya ndege iliyokuwa ikitokea Denver kuelekea Minneapolis Jumapili asubuhi, mwanaharakati Shannon Watts amesema.

Shirika la United limesema wasichana hao walikuwa wanasafiria hati maalum, ambayo hutumiwa na wafanyakazi wa shirika la ndege na wageni wao.

United wamesema huwa kuna kanuni za mavazi kwa wanaotumia hati hiyo kusafiria.

Shirika hilo limefafanua kwamba abiria wa kawaida, ambao wanalipia tiketi zao, wako huru kuvalia mavazi yao ya kubana.

Hati hiyo maalum ya kusafiria ya United huwawezesha walio na hati hiyo kusafiri kwa ndege bila malipo au kwa tiketi za bei nafuu sana.

Kanuni za mavazi kwa wanaotumia hati hiyo hueleza kuwa hawafai kuvalia mavazi ya kubana, iwe ni blauzi za lycra/spandex, suruali ndefu au rinda.

Aidha, hawaruhusiwi kuvalia mavazi yanayoanika vitovu vyao au minisketi.

Mwanaharakati Shannon Watts ameandika kwenye Twitter kwamba kisa hicho kiliathiri wasichana karibu watano waliokuwa wakitaka kuabiri ndege uwanja wa ndege wa Denver.

Alisema wakala mmoja wa United alijaribu kuwashurutisha wasichana hao, mmoja wa umri wa miaka 10, kubadilisha mavazi yao na kuvalia marinda badala ya long'i hizo za kubana.

Alisema wasichana watatu kati ya hao waliruhusiwa kuabiri ndege baada ya kukubali kuvalia marinda, lakini hao wengine wawili walizuiwa kuabiri ndege.



Alishutumu shirika hilo, na kuuliza: "Ni wakati gani United waligeuka na kuwa polisi wa kuamua kuhusu mavazi?"



United baadaye walijibu kwenye Twitter wakisema wenye hati hizo maalum hutakiwa kufuata kanuni maalum za mavazi.



Wanawake wengi wamekuwa wakivaa suruali ndefu za aina hiyo
Wasichana waliovaa nguo za kubana wazuiliwa uwanja wa ndege Marekani Wasichana waliovaa nguo za kubana wazuiliwa uwanja wa ndege Marekani Reviewed by Zero Degree on 3/29/2017 10:28:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.