Loading...

Tengua tengua ya Rais Magufuli yazua mjadala

Hatua ya Rais John Magufuli kutengua uamuzi unaofanywa na wateule wake, imeelezwa kuwa ni dalili ya mpasuko serikalini unaotakiwa kutafutiwa ufumbuzi haraka.

Hali hiyo imejitokeza baada ya Rais Magufuli kutengua uamuzi wa kumshitaki msanii wa muziki wa kizazi kipya, Elibariki Emmanuel maarufu Ney wa Mitego, uamuzi ambao umezua mjadala huku ikielezwa kuwa Rais ameingilia majukumu ya Jeshi la Polisi na Baraza la Sanaa Tanzania (Basata).

Msanii huyo alikamatwa siku chache zilizopita akiwa mkoani Morogoro na kukabidhiwa kwa polisi Mkoa wa Dar es Salaam, ambao walitoa amri ya kumkamata wakidai wimbo wake wa ‘Wapo’ una maudhui yenye kuikashfu Serikali. Akiwa bado mikononi mwa polisi, Basata ilitoa taarifa ya kuupiga marufuku wimbo huo na kuwaonya wananchi wasiendelee kuusikiliza au kuusambaza kwa kuwa ni kosa la jinai.

Hata hivyo, muda mfupi baada ya tangazo la Basata lililosainiwa na Katibu Mtendaji, Godfrey Mungereza, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe naye alitoa tamko akiliagiza Jeshi la Polisi kumuachia huru msanii huyo ikiwamo kuuruhusu wimbo wake.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, Dk Mwakyembe alisema hata Rais Magufuli amefurahishwa na wimbo huo.

Dk Mwakyembe alimshauri msanii huyo kama inawezekana aendelee kutaja watu wengine kama vile wakwepa kodi, wauza unga, wabwia unga, wezi pamoja na watu wengine wasio na maadili mema katika jamii.

Utata na mwingiliano huo wa maagizo umejitokeza ikiwa ni siku chache tangu Rais Magufuli alipofanya mabadiliko madogo ya baraza lake la mawaziri kwa kumtoa Nape Nnauye kwenye nafasi ya uwaziri.

Kauli ya kwanza ya Nape, aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iliyoonekana kutofurahisha mamlaka za juu ni pale alipopinga wasanii waliotajwa ama kuwa na taarifa kuhusu dawa za kuleya, kutumia na kufanya biashara.

Nape alinukuliwa na vyombo vya habari akipinga kitendo cha kuwatuhumu hadharani wasanii hao, kwamba ni kuharibu ‘brand’ zao walizozitengeneza kwa muda mrefu. Muda mfupi kabla ya kung’olewa uwaziri, Nape aliunda kamati kuchunguza uvamizi wa studio za Clouds Media, ambao uliambatana na watu wenye silaha.

Hata hivyo, siku moja baada ya kupokea ripoti ya kamati aliyoiunda kuchunguza tukio hilo, Rais Magufuli alitangaza mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri kwa kumtoa Nape.

Utata kama huo pia ulijitokeza wakati Dk Mwakyembe alipokuwa Waziri wa Sheria na Katiba ambaye Machi 16, 2017 alitangaza kupiga marufuku watu kufunga ndoa bila kuwa na vyeti vya kuzaliwa.

Lakini, Rais Magufuli akiwa Dodoma, alitengua agizo hilo akisema Watanzania wengi hawana vyeti hivyo na kulihitajika maandalizi kabla ya kufikia uamuzi.

Tukio jingine la kukinzana kwa maagizo ni lile la Desemba 6, 2016 ambapo Rais Magufuli alitengua agizo la wakuu wa wilaya za Nyamagana na Ilemela mkoani Mwanza walioagiza wamachinga waondoke katikati ya jiji.

Maoni


Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa chama cha siasa cha Kijamii (CCK), Constantine Akitanda alisema mivutano inayoendelea serikalini ni dalili ya ombwe la uongozi.

“Haya mambo nimekuwa nikiyatafakari na chama chetu pia kimeyaorodhesha yote. Serikali ya Rais Magufuli na wateule wake hawaongei lugha moja, kwa sababu huwezi kutarajia watu wanaofanya kazi Serikali moja watofautiane kiasi hiki,” alisema Akitanda.

Alisema sababu ya kutofautiana huko ni kuacha misingi ya sheria zilizopo.

“Mkishaacha kufuata misingi ya sheria, haya ndiyo yanatokea na bado watahasimiana mno huko tuendako. Wameanza kutofautioana tangu kwenye chama chao, sasa kwenye Serikali. Nape aliamua kujiweka kando na kusikiliza wananchi wanasemaje, akasahau aliyemteua anataka nini,” alisema na kuongeza:

“Tunayo Serikali inayoogopa kukosolewa, inayoogopa vyombo vya habari, inaogopa vyama vya siasa. Hili ni ombwe la uongozi.”

Mchambuzi wa siasa nchini, Dk Ahmed Kiwanuka alisema kukinzana kwa uamuzi kunakojitokeza serikalini ni aina ya utawala na siyo tatizo.

“Rais ni kiongozi mkuu lazima apewe nafasi wakati wowote atoe maelekezo, kwa sababu hawezi akaona mambo yanaharibika halafu anyamaze. Anaweza kupinga kauli ya waziri hadharani ili wengine tujifunze,” alisema na kuongeza:

“Ndivyo tulivyo, wakati mwingine Rais akiingilia mambo wanasema wanabanwa, wakiachwa sana wanaharibu. Inategemea ni kiasi gani. Lakini kwa tukio la karibuni, tunaona Rais halali, anasikiliza hadi wimbo wa ‘Wapo’, anafuatilia,” alisema Dk Kiwanuka.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda alisema kukinzana huko kwa uamuzi kunatokana na nidhamu ya woga ya baadhi ya watumishi wa umma wanaotaka kuwafurahisha wakubwa.

“Kuna tatizo la wateule wanaomsaidia Rais kuwa ‘sensitive’ sana kuliko kawaida. Wanajaribu kupitiliza kimaamuzi ili waonekane kuwa watendaji zaidi. Kuna baadhi ya uamuzi wanatakiwa kufanya utafiti wa kina kabla ya kuuchukua,” alisema.

“Kwa mfano uamuzi alioutoa Dk Mwakyembe ni mkubwa sana kiasi kwamba ulitakiwa ujadiliwe na Baraza la Mawaziri, si yeye peke yake. Tumesikia hivi karibuni kuwa, ili watumishi wa umma wapandishwe madaraja ni lazima wapate mafunzo, huo ni uamuzi mkubwa unaohitaji tafakuri ya kina,” alisema Mbunda.


Source: Mwananchi
Tengua tengua ya Rais Magufuli yazua mjadala Tengua tengua ya Rais Magufuli yazua mjadala Reviewed by Zero Degree on 3/29/2017 10:35:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.