Loading...

Bunge lacharuka sakata la mwalimu mpapasaji watoto


SAKATA la tuhuma dhidi ya mwalimu wa shule ya St. Florence ya jijini Dar es Salaam kuwadhalilisha kingono wanafunzi wake wanne wa kike wa darasa la saba, limelitikisa bunge baada ya wabunge kuitaka serikali ieleze hatua ilizochukua.

Wabunge wa viti maalumu, Ester Mmasi na Zainabu Vulu (wote CCM) wametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Mei 31, 2018 bungeni jijini Dodoma ambapo Mmasi aliyeomba mwongozo wa kiti cha spika, alisema moja ya mikataba ya kitaifa na kimataifa iliyoingiwa na serikali ni kumlinda mtoto asome na kufikia ndoto zake, lakini kumekuwa na viashiria vya kukosa ulinzi hasa kwa mtoto wa kike.

“Kupitia mitandaoni, wazazi wameripoti kuwa mwalimu anayeitwa Ayubu Mlugu wa Shule ya St Florence ya Dar es Salaam, kuna vitendo viovu anavyowafanyia watoto wao, ameshtakiwa na walimu wenzake na wanafunzi, lakini mkuu wa shule hiyo alizuia taarifa zisifikishwe serikalini wala wazazi wa watoto hao. Mpaka sasa amewaathiri kisaikolojia watoto wanne. Serikali iseme ni lini itawalinda watoto hawa waweze kusoma kwenye mazingira tulivu?” amesema Mmasi.

Naye Vulu alisema: “Ninasikitika na nina majonzi makubwa sana, nataka kujua ni lini serikali itachukua hatua, hawa watoto bado wadogo tena wa kike, wameathirika kisaikolojia. Picha zinasambaa mitandaoni na sheria ipo ya kuwalinda watoto.”

Baada ya maswali hayo, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, alieleza kwamba miongozo ya wabunge hao wawili inazungumzia matukio ambayo hayajatokea mapema leo, kwa mujibu wa kanuni za bunge, lakini kwa kuwa ni tukio la kusikitisha, kufadhaisha na kuudhi, Chenge aliipa fursa serikali kuyatolea ufafanuzi.

Akitoa ufafanuzi kwa niaba ya serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama, amesema serikali imesikia kutoka kwa wabunge lakini hata yenyewe imepata ukakasi kutokana na tukio hilo baya, huku akieleza kuwa serikali inahitaji kulifanyia kazi ya kina, na kuomba kupewa nafasi ya kulichunguza jambo hilo kabla ya kutoa maelezo bungeni.

Inadaiwa baadhi ya wazazi wa watoto anaosoma katika shule hiyo wameanza kuwahamisha watoto wao huku wenye watoto wa darasa la saba wakishindwa kufanya hivyo kutokana na muda mfupi uliobaki kwa watoto hao kufanya mtihani wa taifa wa kuhitimu elimu ya msingi.
Bunge lacharuka sakata la mwalimu mpapasaji watoto Bunge lacharuka sakata la mwalimu mpapasaji watoto Reviewed by Zero Degree on 5/31/2018 04:48:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.