Loading...

Mauaji mapya ya kishirikina yazuka Mbeya


JINAMIZI la mauaji na ubakaji wa watoto wadogo kutokana na imani za kishirikina, limeikumba wilaya ya Chunya mkoa wa Mbeya. Hali hiyo imeilazimu serikali ya mkoa wa Mbeya kutoa tamko na kuiagiza kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, kuchukua hatua madhubuti.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amosi Makalla alisema hayo katika mkutano wa hadhara na wakazi wa Kijiji cha Kiwanja Kata ya Mbugani wilayani Chunya. Alisema matukio ya ubakaji na mauaji ya watoto wilayani hapa, yamekithiri na chanzo ni imani za kishirikina. Makalla alisema katika siku za hivi karibuni, wapo watoto watatu waliobakwa na kuuawa wilayani hapo, ambapo mmoja alikuwa na umri wa miezi tisa mwingine miezi saba na wa tatu alikuwa na miezi mitatu.

Alisema matukio hayo yote, yanaonekana kuhusishwa na imani za kishirikina, ambapo wahusika wa matukio hayo, wanadaiwa kuaminishwa na waganga wa jadi kuwa iwapo watafanya vitendo hivyo, watapata utajiri kwa kupata madini ya dhahabu kwenye maeneo ya migodi, wanakofanyia shughuli zao. Makalla aliagiza kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Chunya, ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya, Rehema Madusa kukaa na viongozi wa vijiji haraka iwezekanavyo na kuchukua hatua dhidi ya watu wanaojihusisha na vitendo hivyo na waganga wanaowaaminisha ujinga huo.

Mkuu wa Mkoa alisema serikali haitafumbia macho suala hilo. Kwamba iwapo vitendo hivyo vitaendelea, ataendesha upigaji kura za siri kwa kuwa anaamini wananchi wanawatambua watu wanaojihusisha na matukio hayo, ingawa wanasita kuwataja hadharani. “Hatutaleta lambalamba hapa, ila tutatumia njia ambazo lazima watajulikana tu.

Acheni haya mambo, hayana manufaa kwa Chunya yenu! Mnadanganywa eti ukibaka au ukiua mtoto utapata dhahabu. Huo ni uongo mtupu,”alisisitiza. Makala alisema hivi karibuni kulikuwa na watu wanaojiita Wakorea Weusi. “Tulifanya kazi tukapata mpaka kiini chao. Sasa ninyi mnaojihusisha na vitendo hivi msifikiri, hatuwezi kuwapata nawahakikishia tutawapata tu na dawa yenu mtaipata,” alisema.

Source: Habari Leo
Mauaji mapya ya kishirikina yazuka Mbeya Mauaji mapya ya kishirikina yazuka Mbeya Reviewed by Zero Degree on 5/31/2018 04:50:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.