Mbowe alia siasa mazishi ya Bilago
KATIKA hali isiyo ya kawaida, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na uongozi wa Bunge wamejikuta wakitoleana maneno 'mazito' msibani kutokana na kile kilichodaiwa upande mmoja kutotendewa haki na upande wa pili.
Hali hiyo ilitokea jana bungeni jijini Dodoma wakati wa kuagwa kwa mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Buyungu mkoani Kigoma, Kasuku Bilago (Chadema).
Baada ya kumaliza kwa misa ya kuaga mwili huo, ulifuata utaratibu wa viongozi wa serikali, Bunge na vyama vya siasa kutoa neno, ndipo Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alipotumia nafasi hiyo kulitaka Bunge kuacha alichokiita siasa katika mazishi ya mwanachama wao huyo.
Huku kauli yake ikipingwa vikali na Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, baadaye Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa, aliutaka uongozi wa Bunge kuichia familia na chama kuamua siku ya kuzikwa mwili wa Bilago kwa jinsi wanavyotaka.
Mbunge huyo wa Hai mkoani Kilimanjaro, alisema familia na wananchi wa Jimbo la Buyungu wana haki ya kuuaga mwili wa aliyekuwa mbunge wao, hivyo Bunge kutaka uzikwe leo badala ya Alhamisi wanavyotaka Chadema na familia, kutawanyima fursa hiyo.
"Familia na wapigakura wake wana haki ya kumzika mpendwa wao. Naomba tuache 'ku-politicize' (husisha na siasa) mazishi haya. Tumepeana mikono ya amani hapa, amani hii isiwe ya kinafiki," Mbowe alisema.
Aliongeza kuwa Chadema wangependa kumzika kuuzika mwili wa marehemu Jumamosi, lakini familia imekaa na kuamua kumzika Alhamisi, lakini Bunge limesema utazikwa Jumatano (leo).
Mbowe alisema ni jambo la ajabu kuona Chadema wametoa ratiba ya mazishi lakini Bunge likaja na ratiba yake tofauti.
Alisema Bunge haliwezi kupokea mamlaka ya familia na chama hivyo akataka uamuzi wa familia uheshimiwe kuhusu siku ya kuzikwa kwa mwili wa mpendwa wao.
Aliongeza kuwa msiba huo ni mzito kwa familia na Chadema kwa kuwa Bilago alikuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Magharibi (Tabora, Katavi na Kigoma) na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.
Mbowe pia alisema kifo cha mbunge huyo kinapaswa kitumike kuleta upatanisho na kutafakari maisha ya binadamu kila siku, lakini akabainisha kuwa umoja na mshikamano wa wabunge ulioonekana wakati wa kuagwa kwa mwili huo haumo ndani ya Bunge.
Alisema utukufu na vyeo vyote mwisho wake ni kifo, hivyo hakuna sababu ya kuumizana wao kwa wao.
NAIBU SPIKA AJIBU
Kutokana na kauli nzito hiyo ya Mbowe, Naibu Spika (Dk. Tulia) alilazimika kutoa ufafanuzi, akieleza kuwa Bunge halina sababu ya kupoka madaraka ya familia kuhusu mazishi hayo.
Alibainisha kuwa awali Kamati ya Uongozi ya Bunge iliketi Jumapili saa tano asubuhi pamoja na Tume ya Utumishi ya Bunge na wakaafikiana kuwa mazishi yafanyike Jumatano ((leo).
Dk. Tulia alisema Mbowe ambaye ni mjumbe katika Kamati ya Uongozi, hakuwapo katika kikao hicho cha Jumapili kwa kuwa alikuwa Dar es Salaam, lakini aliwakilishwa.
Alibainisha kuwa taarifa za kuwa mazishi yatafanyika Alhamisi zilifika baada ya kamati hiyo kukaa.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa Bunge alisema halijaharibika jambo kwa kuwa kila kitu kitakwenda jinsi chama, uongozi wa familia na Bunge wamejipanga.
Alimtaka Mbowe kuondoka kwa amani bungeni jana kwa kuwa wakifika Kigoma, atakutana na Spika Job Ndugai na anaamini hakutaharibika neno.
Dk. Tulia aliweka wazi kuwa taarifa za msiba wa mbunge huyo walizipokea kwa mshtuko mkubwa na wabunge wengi walikuwa hawajui kama anaumwa.
Alisema kuwa huyo ni mbunge wa nne kufariki dunia katika Bunge la 11 na msiba huo 'umewapiga' sana wabunge wote.
Bilago alizaliwa miaka 54 iliyopita na ameacha mke na watoto watatu.
Aliwahi kufanya kazi ya ualimu kwa zaidi ya miaka sita na alikuwa Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM kabla ya kujiunga na Chadema.
Alifariki dunia Jumamosi kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa anapatiwa matibabu ya kibingwa.
Awali wakati wa kuaga mwili wa Bilago, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, ambaye jana alikuwa anakaimu nafasi ya Waziri Mkuu bungeni, alitoa salamu za rambirambi kutoka kwa Rais John Magufuli na kueleza kuwa Bunge limepoteza mbunge mahiri aliyekuwa anatoa michango mizuri.
"Kifo ni jambo ambalo haliepukiki kwa binadamu. Sisi sote ni wasafiri, duniani tunapita tu. Poleni sana familia, poleni Bunge na chama chake," alisema Dk. Mwinyi.
Wawakilishi wa wabunge wa CCM, Venance Mwamoto na CUF, Salim Hussein na NCCR-Mageuzi, James Mbatia, waliwataka wabunge wenzao kuutumia msiba huo kutafakari mienendo yao duniani kwa kuwa hawajui saa wala siku ya kufa kwao.
Naye Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), alisema Bunge na nchi imepata pigo kwa kuondokewa na mbunge mahiri wakati anachangia hoja bungeni kila mbunge alilazimika kuacha alichokuwa anakifanya ili kumsikiliza.
Source: Nipashe
Mbowe alia siasa mazishi ya Bilago
Reviewed by Zero Degree
on
5/30/2018 09:05:00 AM
Rating: