Loading...

Kakonko kinara kwa maambukizi ya Malaria


RIPOTI ya utafiti wa kina wa viashiria vya malaria nchini kwa mwaka 2017 iliyoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imetaja halmashauri za Kakonko, Kasulu, Kibondo, Uvinza, Kigoma, Buhigwe, Geita, Nanyamba, Muleba na Mtwara kuwa ndio vinara wa maambukizi ya ugonjwa huo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo Dar es Salaam jana, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema Halmashauri ya Kakonko (DC) inaongoza kwa kiwango cha asilimia 30.8 ikifuatiwa na Halmashauri ya Kasulu yenye asilimia 27.6.

Alitaja nyingine zinazofuata ni Kibondo (DC) asilimia 25.8, Uvinza (DC) asilimia 25.4, Kigoma (DC) asilimia 25.1, Buhigwe (DC) asilimia 24, Geita (DC) asilimia 22.4, Nanyamba (TC) asilimia 19.5, Muleba (DC) asilimia 19.4 na Mtwara (DC) asilimia 19.1.

Alisema halmashauri zenye kiwango kidogo chini ya asilimia sifuri ni Mbulu (TC), Mbulu (DC), Hanang, Hai, Siha, Moshi, Mwanga, Kondoa (TC), Meru (DC), Arusha (CC), Arusha (DC), Monduli, Ngorongoro na Rombo (DC).

“Aprili mwaka huu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani baada ya kuzindua ripoti ya utafiti wa viashiria vya malaria nchini ya mwaka 2017, ambayo inaonesha kiwango cha maambukizi ya malaria kitaifa kimepungua kutoka asilimia 14.4 mwaka 2015 hadi asilimia 7.3 mwaka 2017/18.

“Pamoja na hayo, niliwaagiza NBS kuandaa ripoti nyingine inayoeleza kwa kina kiwango cha maambukizi kwa kila halmashauri ninayoizindua leo (jana), lengo letu tunataka kujua hali ilivyo kila halmashauri ili tuwekeze nguvu zaidi katika kukabili ugonjwa huu,” alisema.

Alisema matokeo ya utafiti huu yanaeleza asilimia 78 ya kaya nchini zinamiliki angalau chandarua kimoja chenye dawa, kiwango hicho kimepanda ikilinganishwa na asilimia 66 ilivyokuwa mwaka 2015-16.

“Umiliki wa vyandarua vyenye dawa ni wa kiwango cha juu kwa kaya za mijini kwa asilimia 81 ikilinganishwa na kaya za vijijini asilimia 77,” alisema.

Alisema kwa upande wa Tanzania Bara, Mkoa wa Pwani unaoongoza kuwa na kiwango kikubwa cha umiliki wa vyandarua vyenye dawa (asilimia 89) na Njombe una kiwango kidogo cha asilimia 58 ikilinganishwa na mikoa mingine.

“Zanzibar, Mkoa wa Kusini Pemba una kiwango kikubwa cha umiliki wa vyandarua vyenye dawa asilimia 90 na mkoa wenye kiwango kidogo cha umiliki ni Mjini Magharibi asilimia 73,” alisema.

Alisema matokeo hayo yatawasilishwa kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Seleman Jafo ili kuanza utekelezaji.

“Nitamkabidhi Jafo ili aingie mkataba na wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha wanakwenda kusimamia utekelezaji wake, atlas hii itakuwa ndiyo kipimo chao.

“Lakini nitoe rai pia kwa mabibi na mabwana afya, badala ya kupoteza muda kupita kwenye migahawa na mabucha kwa sababu huko wanakusanya mapato, wanapata ‘ten parcent’, sasa waanze kupita kwenye mitaa, kaya kuhamasisha jamii kufanya usafi wa mazingira ili kuongeza nguvu ya kukabiliana na maambukizi ya malaria katika halmashauri zao na taifa kwa ujumla,” alisema.

Alisema sambamba na hilo, Serikali inakusudia kuanza kununua vitendanishi (vipimo) vya malaria na kuvisambaza kote nchini ili kila raia aweze kujipima mwenyewe iwapo ana malaria au la.

“Ni suala ambalo hatujafikia mwafaka, tupo kwenye majadiliano na wadau wetu wa maendeleo Global Fund,” alibainisha.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa alisema matokeo hayo yatasaidia watunga sera kuweka mikakati madhubuti ya kuukabili ugonjwa huo.

“Hii ni mara ya kwanza kwa NBS kuandaa atlas hii, lengo ni kuwapatia watunga sera, wanasiasa na wadau wa maendeleo hali halisi ya kiwango cha maambukizi ya malaria katika ngazi ya halmashauri.

“Ni vema pia wakazingatia kuyachambua matokeo haya kwa manufaa ya taifa, lakini si kukosoa. Kama wana maoni waje tutajadiliana,” alisema.

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, Salma Kikwete alisema halmashauri hizo zinapaswa kujipanga.

“Hawa waliofanya vibaya wajipange, inawezekana kutokomeza malaria mbona Zanzibar wameweza, kila mmoja awajibike katika eneo lake,” alisema.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Peter Selukamba alisema matokeo hayo yatasaidia nchi kupata sera madhubuti zitakazosaidia kutokomeza ugonjwa huo.

“Hatuna budi sasa katika mwaka wa fedha 2019/20 kuangalia namna gani tutafikia lengo, tujikite sasa katika kuangamiza mazalia ya mbu, ni vema pia kila halmashauri ikaunda sheria ndogo ndogo kuhakikisha kunakuwa na ufuatiliaji kila kaya itumie chandarua na kusimamia ipasavyo usafi wa mazingira,” alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge Kinachopambana na Maambukizi ya Malaria, Riziki Lulida alishauri Serikali kutunga sheria itakayoelekeza mashimo katika maeneo ya migodi kufunikwa pale shughuli za uchimbaji zinapokamilika na migodi kufungwa.
Kakonko kinara kwa maambukizi ya Malaria Kakonko kinara kwa maambukizi ya Malaria Reviewed by Zero Degree on 10/24/2018 08:35:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.