Loading...

TRA kusaka wakwepa kodi nchi nzima


ZIKIWA zimepita siku tano tangu ilipoanza operesheni kali ya kukamata wanaoghushi risiti za kielektroniki (EFD) Kariakoo jijini Dar es Salaam, sasa imeanza kufanyika nchi nzima.

Maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) wanafanya msako mkali kubaini wanaoiibia Serikali.

Hatua hii inakuja siku chache tu tangu gazeti hili lilipochapisha ripoti maalumu iliyonesha jinsi baadhi ya wafanyabiashara katika eneo la Kariakoo wanavyoiibia serikali.

Aidha, kupitia operesheni hiyo, mamlaka hiyo imesema kuwa watakaokamatwa watalipa faini, kufungwa jela au mizigo yao kutaifishwa.

Katika operesheni kali inayoendelea katika eneo la Kariakoo ambapo baadhi ya wafanyabiashara na wateja wao walikamatwa na risiti feki huku wengine wakikutwa wakiuza bidhaa bila kutoa risiti.

Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Mlipa Kodi mamlaka hiyo, Richard Kayombo aliliambia gazeti hili kuwa mamlaka hiyo imeamua kuifanya operesheni hiyo kitaifa na iwapo yeyote atabainika, hatua kali zitachukuliwa.

Alisema,"Tulianza na operesheni juzi (Jumatano) katika eneo la Kariakoo lakini sasa inahamia nchi nzima, haiwezekani watu wakakiuka sheria tukawavumilia huku serikali ikipoteza mapato.

"Tunaendelea kutoa elimu juu ya faida ya kulipa kodi lakini kuna wasiowaaminifu ambao wanaiba tena kwa kughushi risiti... "...wengine wanatoa risiti ambazo hazielezi thamani halisi iliyotolewa na mteja lakini pia wengine wanatumia risiti moja kusafirisha mizigo tofauti kwa nyakati tofauti," alisema Kayombo na kueleza kuwa maofisa wa mamlaka hiyo kwenye mikoa mingine ya Kodi wanaendelea na kazi hiyo.

Aidha, alitoa tahadhari kuwa wanaofanya hivyo kuwa wakikamatwa watalipa fidia kubwa, kufungwa jela au hata bidhaa zao kutaifishwa.

Alisema,"Tukikubaini, lazima ulipe faini au faini na kifungo. Na kama mzigo wako utakamatwa basi tutauchukulia kuwa ni mzigo usiokuwa na mwenyewe kwani risiti halisi ya TRA ndiyo utambulisho wa mzigo iwapo umenunuliwa."

Katika mji wa Babati mkoani Manyara, mfanyabiashara Isaac Mushi ambaye anafanya biashara ya vifaa vya umeme alisema kuwa maofisa hao wamefika kwenye eneo lake la biashara na kuchunguza iwapo risiti za EFDs zinazotolewa zinakabidhiwa na kutumika kwa usahihi na kwamba juhudi hizo ni nzuri kwa faida ya taifa.

Alisema, "Nilisoma kwenye gazeti la HabariLeo Jumatatu iliyopita, liliandika kuhusu jinsi walipa kodi wanavyoiibia Serikali. Kwa kweli kama mfanyabiashara nilisikitika kwani hao wanaofanya hivyo wanafanya kuhujumu maendeleo ya nchi.

"Ni kweli kila mfanyabiashara anataka faida, tena iliyo kubwa lakini tunapaswa kutambua kuwa Serikali nayo inahitaji fedha kwa ajili ya kuleta maendeleo kama barabara na umeme.

"Maendeleo hayo yakishaletwa, na sisi kazi inakuwa rahisi, uwezekano wa kuongeza kipato unakuwa mkubwa," alisema mfanyabiashara huyo aliyezungumza kwa njia ya simu huku akiipongeza mamlaka hiyo ya mapato kwa kile inachokifanya.

Yohana Maduhu ambaye ni mfanyabiashara mwenye duka la vinywaji katika mtaa wa Uhuru jijini Mwanza alisema kuwa maofisa wa TRA hufika mitaa hiyo mara kwa mara kwa ajili ya ukaguzi, jambo ambalo linaashiria uwajibikaji.

Maduhu alisema, "Awamu hii, watu wanafanya kazi, lakini hili suala la kodi niseme tu ni kwamba tunalipa. Kama wako wanaodanganya basi watakamatwa kwani serikali ina mkono mrefu na inaweza kuwabaini wote wanaofanya kinyume na utaratibu."

Mmoja wa wafanyabiashara mkoani Mbeya, Aristus Nonga aliliambia gazeti hili kuwa hajashuhudia ukaguzi unaofanywa kwenye mkoa huo isipokuwa ana taarifa kuwa kuna maofisa wanaoshtukiza kwenye maduka na kwamba zoezi hilo limetiliwa mkazo baada ya kubainika kuwepo kwa wafanyabiashara Kariakoo ambao wamekithiri.
TRA kusaka wakwepa kodi nchi nzima TRA kusaka wakwepa kodi nchi nzima Reviewed by Zero Degree on 10/29/2018 09:35:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.