Loading...

Kiongozi wa upinzani azuiwa kusafiri, akaunti zake zazuiwa


MAHAKAMA ya Rufaa nchini Venezuela imemzuia kiongozi wa upinzani nchini humo, Juan Guaidó kuondoka nchini na kuamuru akaunti zake za benki zizuiwe.

Mahakama ambayo inamuunga mkono Maduro, imetoa uamuzi huo baada ya Mwanasheria Mkuu, Tarek William Saab kuitaka kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya Guaido. Kiongozi wa mahakama, Maikel Moreno alisema mahakama imemzuia Guaido kuondoka nchini hadi hapo uchunguzi wa awali utakapokamilika. Hatua hiyo inatokana kile kinachoelezwa kuwa amesababisha uvunjifu wa amani katika nchi.

Akiwa kiongozi wa bunge, Guaidó ana kinga ya kushitakiwa isipokuwa kwa uamuzi wa mahakama ya juu. Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufika bungeni, kiongozi huyo wa upinzani alisema haoni kipya. “Sitaacha kumkabili (Maduro)…tunaendelea na kazi yetu,” alisema.

Uamuzi wa mahakama umekuja muda mfupi baada ya Marekani kusema imemkabidhi Guaido mamlaka ya kudhibiti akaunti za benki za Venezuela kwa kuwa ndiye wanayemtambua kuwa rais wa mpito. Katika ukurasa wa tweeter wa Mshauri wa masuala ya usalama wa Marekani, John Bolton, alisema watawakabili wanaojaribu kupindua demokrasia na kumdhuru Guaidó.

Guaidó anataka urais kwa kile anachodai kwamba akiwa kiongozi wa bunge, katiba inamruhusu kushika madaraka ya mpito endapo rais anaonekana kutokuwa halali. Mzozo huo wa kugombea madaraka ulikuwa mkubwa baada ya hivi karibuni kiongozi huyo wa upinzani kujitangaza kuwa rais wa mpito. Guaido anaungwa mkono na Marekani, Canada, Brazil, Colombia na Argentina na Muungano wa Ulaya ambao unataka uchaguzi ufanyike upya. Kwa upande wa Rais Nicolas Maduro anaungwa mkono na baadhi ya mataifa ikiwamo Urusi na China.

Awali, Urusi kupitia wizara yake ya mambo ya nje ilionya kuwa hatua ya Guaido kujitangaza kuwa rais ingesababisha uvunjaji wa sheria na umwagikaji mkubwa wa damu. Kwa upande wake, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China, Hua Chunying, alisema nchi yake inapinga vitendo vya mzozo huo wa kisiasa kuingiliwa na mataifa ya nje. Alisema China inaunga mkono mikakati ya Venezuela ya kulinda uhuru wake wa kujitawala. Uturuki pia imemhakikishia Maduro kuwa itakuwa pamoja naye na ikamtaka asimame imara.

Alipohojiwa na waandishi wa habari, Rais Maduro alisema yuko tayari kwa ajili ya majadiliano na upinzani. “Niko tayari kukaa meza moja na upinzani ili tuzungumze kwa ajili ya ustawi wa Venezuela,” aliliambia shirika la habari la Urusi la RIA Novosti lililopo mjini hapa. Hivi karibuni, Rais Maduro alisimamisha uhusiano wa kisiasa kati ya nchi yake na Marekani baada ya Rais Donald Trump kumtambua Guaido kama kiongozi wa muda wa Venezuela.
Kiongozi wa upinzani azuiwa kusafiri, akaunti zake zazuiwa Kiongozi wa upinzani azuiwa kusafiri, akaunti zake zazuiwa Reviewed by Zero Degree on 1/31/2019 02:05:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.