Loading...

Tanzia: Mvumbuzi tanzanite afariki dunia


MVUMBUZI wa madini ya tanzanite, Mzee Jumanne Ngoma (85), amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN) muda mfupi baada ya kufikishwa hapo.

Aprili 6, mwaka jana, Rais John Magufuli, alitangaza kumtambua Mzee Ngoma kuwa ndiye mvumbuzi wa madini hayo na alimpatia Sh. milioni 100, ili zimsaidie kwenye matibabu kutokana na maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.

Rais Magufuli alitangaza kumtambua mzee huyo akiwa mji mdogo wa Mirerani ulioko Simanjiro mkoani Manyara, wakati akizindua ukuta uliozunguka machimbo ya madini ya tanzanite, uliojengwa na kikosi cha majeshi ya ulinzi.

Kwa mujibu wa gazeti la Nipashe, mtoto wa marehemu, Hassan Ngoma, alisema baba yake alifariki dunia siku hiyo baada ya kufikishwa chumba cha dharura akitolewa Hospitali ya Boch iliyoko Kimara jijini Dar es Salaam.

Hassan alisema baba yake alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya kiharusi.

“Baba yetu alilazwa jana (juzi) Hospitali ya Boch, Kimara na ilipofika mchana alihamishiwa Muhimbili, lakini wakati akiwa chumba cha dharura Muhimbili majira ya saa 7:00 mchana alifariki dunia,” alisema.

Hassan alisema wakati huo akizungumza na gazeti hili walikuwa wamemaliza taratibu za kumhifadhi kwenye chumba cha kuhifadhia maiti hospitalini hapo.

“Utaratibu unaofuata hivi sasa ni kwamba jioni ya leo (jana) tutakuwa na kikao kitakachofanyika kwa kaka yetu mkubwa huko Mbezi Kimara, ambacho kitaamua lini atasafirishwa kwa ajili ya mazishi kama unavyojua mzee wetu alipewa heshima kubwa na Rais Magufuli baada ya kutambuliwa kuwa ndiye mvumbuzi wa tanzanite,” alisema.

Baada ya Rais Magufuli kumkabidhi mzee Ngoma fedha hizo zilitumika kwa ajili ya matibabu, ambapo alipelekwa nchini India na baadaye kurejea Tanzania.

Alipokuwa akizindua ukuta wa Mirerani uliojengwa kwa Sh. 5,645,843,163, Rais Magufuli aliahidi kuandika barua maalum ya kumtambua Mzee Ngoma.


Akizungumza kwenye hafla hiyo, Rais Magufuli, alisema alipata ujumbe mfupi na baadaye kupata taarifa kutoka kwa mtoto wake, Hassan Ngoma na alipofuatilia alibaini ni za kweli.

“Nimeambiwa tangu mwaka 1967 madini haya yaligunduliwa na mzee huyu, lakini pamoja na kutambuliwa na Rais wa Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, kwenye barua niliyoiona iliyosainiwa tangu tarehe 3/8/1980 na nakala yake ya kuvumbua madini ya aina ya pekee na kuyapeleka kwa mtaalamu wa madini na miamba mwaka 1967, barua hiyo nayo ninayo hapa,” alisema Rais Magufuli wakati huo.

Aliongeza kuwa: “Hii inadhihirisha tanzanite haijavumbuliwa na mtu kutoka nje, nimeambiwa mzee huyu hivi sasa amepooza kidogo,” alisema.

Magufuli alisema barua ya mtaalamu wa madini aliitia saini Septemba 23, 1967 na alishatia saini hati ya kupewa tuzo ya sayansi ya ufundi mwaka 1984.

Alisema licha ya kuvumbua madini hayo, lakini mzee huyo amekuwa akihangaika siku nyinyi tangu mwaka 1967.

“Ukifanya chochote hata kama ni kizuri namna gani, hata ungegundua nini, ninafahamu wagunduzi wengi chuo kikuu lakini hawakutambuliwa, hata mimi niligundua kitu fulani cha Kemia, lakini nilivyoomba kutambuliwa mpaka leo wamebaki na kitabu changu kwenye Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,” alisema na kuongeza:

“Nimeona nimlete hapa ili Watanzania wamtambue, ili kusudi akatibiwe vizuri, serikali itampa Sh. milioni 100 ili akazitumie katika matibabu yake na kujisitiri mambo mengine, fedha hii itawekwa kwenye akaunti yake kesho au kesho kutwa zimsaidie.”
Tanzia: Mvumbuzi tanzanite afariki dunia Tanzia: Mvumbuzi tanzanite afariki dunia Reviewed by Zero Degree on 1/31/2019 09:05:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.