Loading...

Mahabusu walala kwa zamu Mpanda


Mahabusu waliopo katika Gereza la Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi wanalazimika kulala kwa zamu kutokana na gereza hilo kuzidiwa na msongamano wa wafungwa na mahabusu.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Katavi, Emmanuel Ngigwana alisema hayo jana wakati wa kilele cha Siku ya Sheria, iliyofanyika kwenye viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Mpanda.

Alisema kutokana na gereza hilo kuzidiwa, mahabusu hulazimika kulala kwa zamu akimaanisha wakati wengine wakiwa wamelala, wenzao hulazimika kukaa au kusimama.

Imeelezwa kuwa gereza hilo lina uwezo wa kuchukua mahabusu 100, lakini walipo ni zaidi ya 400.

Hakimu huyo alisema umefika wakati kwa uongozi wa mkoa kuanza kufikiria kujenga gereza mahsusi kwa mahabusu katika Wilaya ya Mlele kwa kuwa haina gereza na mahabusu wake hupelekwa Gereza la Mpanda hali inayosabababisha msongamano huo.

Alisema kwa kuzingatia hali ya jiografia ya Mkoa wa Katavi, kusafirisha mahabusu kutoka Gereza la Mpanda hadi Mahakama ya Wilaya ya Mlele kuna umbali wa kilomita zaidi ya 100 na wengi ni wale wanaoshtakiwa kwa kesi za mauaji na uhujumu uchumi, jambo ambalo alisema ni hatari ikizingatiwa umbali huo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Amos Makalla alisema kuwapo kwa msongamano wa mahabusu na wafungwa katika gereza hilo ni tatizo na tayari wameshaanza kuchukua hatua kwa kuwasiliana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambako kimsingi wamekubaliana kuanza ujenzi wa gereza la mahabusu katika Wilaya ya Mlele.

Makalla alisema ujenzi huo utafanywa na wizara hiyo kwa kushirikiana na mkoa ili kumaliza changamoto hiyo.

Mkuu wa ofisi ya mashtaka wa Mkoa wa Katavi, Elisante Masaki alivipongeza vyombo vya habari kwa kuibua tatizo hilo na kuomba viendelee kuwa sauti ya umma kwa kuibua matukio yote yasiyo ya kiungwana katika jamii ili yashughulikiwe na vyombo husika.

Hata hivyo, alisema pamoja na kazi nzuri ya vyombo vya habari, alivitaka vikumbuke kuzingatia weledi katika taaluma yao na vijiepushe kuingilia uhuru wa Mahakama kwa kutolea uamuzi mashauri yaliyopo kortini.

Chanzo: Mwananchi
Mahabusu walala kwa zamu Mpanda Mahabusu walala kwa zamu Mpanda Reviewed by Zero Degree on 2/08/2019 07:10:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.