Loading...

IGP Sirro aeleza siri ya askari wake kuendelea kubaki Kibiti

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini(IGP), Simon Sirro
MKUU wa Jeshi la Polisi nchini(IGP), Simon Sirro jana alieleza siri ya askari wake kuendelea kuwapo katika wilaya ya Kibiti mkoani Pwani licha ya eneo hilo lililokuwa limegubikwa na mauaji mfululizo ya watu wasio na hatia kutulia kwa muda mrefu.

IGP Sirro ambaye ukomeshaji wa mauaji ya raia Pwani ilikuwa moja ya ahadi zake baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo Mei 29, mwaka huu, alisema Polisi inaendelea na operesheni ya usalama katika eneo hilo ili kutokomeza kabisa uhalifu uliokuwa ukifanyika.

Sirro alitoa kauli hiyo jana alipopewa nafasi ya kusalimia waumini alipohudhuria ibada ya pili kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, mjini Dodoma.

Alisema kwasasa Kibiti ni shwari lakini Jeshi la Polisi linaendelea na operesheni kuhakikisha mauaji yaliyoigubika kwa zaidi ya mwaka mmoja hayatokei tena.

Watu 40, wakiwamo askari polisi 15, waliripotiwa kuuawa kwa kupigwa risasi Kibiti na wilaya za Mkuranga na Rufiji mkoani Pwani tangu mauaji hayo yalipoanza mwaka 2015.

Aidha, akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuanza ziara ya kikazi mkoani Mtwara Oktoba 4, mwaka huu, IGP Sirro alisema baadhi ya wahalifu kutoka maeneo hayo ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji walikuwa wamekimbilia mkoani humo na kwamba askari wake walikuwa wakiendelea kuwasaka kwa nia ya kupambana nao.

Akiwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba jana, Sirro alisema awali ilikuwa vigumu wananchi kuamini kwamba Kibiti, Rufiji na Mkuranga ni shwari lakini anawahakikishia kuwa eneo hilo ni salama na kila mmoja anaweza kwenda.

Alisema hakuna sababu ya mtu yeyote kuhofia kwa sababu usalama upo na mauaji yamekwisha.

IGP Sirro alisema lengo la Polisi ni kuona wakazi wa Kibiti wanaishi bila hofu yoyote kutokana na ulinzi kuimarishwa na kwamba jeshi lake lipo imara na limefanikiwa kudhibiti uhalifu uliokuwa katika eneo hilo.

Alisisitiza wananchi kuendelea kutoa taarifa pindi watakapoona kuna uhalifu kwenye eneo hilo na maeneo mengine.Alisema pia jeshi hilo limejipanga kupambana na wahalifu ambao watajitokeza katika maeneo yote nchini.Akiwa mjini Mtwara, IGP Sirro alisema:

"Mimi niliwaambia (majambazi) hakuna salama katika Tanzania labda wakimbilie sehemu nyingine."Lakini Mtwara ipo Tanzania. Ukienda Lindi, bado ipo Tanzania.  

"Tutawafuata huko waliko na tutawagonga (tutawapiga) vizuri kwa mujibu wa sheria kwa sababu wao ndiyo wameanzisha ligi (uhalifu). 

"Ukianzisha ligi jitahidi kumaliza ligi." Aliwaambia majambazi hao waliokuwa Kibiti kwamba suala la kukimbia bado haliwasaidii. 

Alisema cha msingi ni majambazi hao kuacha vitendo vya ovyo ovyo ili warudi wawe Watanzania wazuri na Tanzania itawasaidia ipasavyo. KULIPA KISASIMapema mwaka huu IGP Sirro alikiambia kituo cha Radio One kuwa uchunguzi wa polisi ulibaini wauaji walikuwa wanalipa kisasi kwa kile alichodai hisia za kutotendewa haki na baadhi ya watendaji wa serikali na maofisa wa jeshi hilo.

IGP Sirro alisema ilichukua muda mrefu kwa jeshi hilo kukabiliana na wahusika wa mauaji hayo kutokana na wauaji kujipenyeza ndani ya jamii ya wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji kwa karibu muongo mmoja, hivyo kuwa sehemu ya wakazi maeneo husika.

"Waliingia kwenye maeneo hayo (Kibiti, Mkuranga na Rufuji) miaka nane kabla ya kuanza mauaji," IGP Sirro alisema. "Walijipenyeza kwa njia mbalimbali ... unadhani wanaendesha mafunzo ya kidini kumbe kinachofanyika ni mambo tofauti kabisa. 

"(Wauaji) waliwapotosha watu kwamba 'elimu mnayopewa hii haina maana'. Wakafundisha karate, judo na namna ya kutumia silaha." 

Alisema operesheni ilivyofanywa kwenye maeneo husika imefanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa kadhaa wa mauaji hayo, lakini baadhi yao walikimbilia maeneo mengine ya nchi.

Baadhi ya watu waliouawa katika wilaya hizo za mkoa wa Pwani ni pamoja na Ramadhani Mzuzuri (45), mkazi wa Ruaruke wilayani Kibiti aliyeuawa kwa kupigwa risasi nane nyumbani kwake usiku wa kuamkia Julai 10, mwaka huu.Wauaji pia walimjeruhi mke wake, Halima Mzururi kwa kumpiga risasi tatu.

Aprili, askari nane waliokuwa kwenye gari la polisi wakitoka kubadilishana lindo walishambuliwa na majambazi na saba waliuawa kwa risasi huku mmoja akijeruhiwa, katika eneo la Mkengeni, Kata ya Mjawa wilayani Kibiti.

GENGE LA WAUAJI Agosti 10, IGP Sirro alitangaza jeshi hilo kuwaua watuhumiwa 13 wa genge la mauaji katika wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji.

Waliouawa, alisema, ni Hassani Ali Njame, Abdallah Abdallah Mbindimbi maarufu kama Abajani, Saidi Abdallah Kilindo, Abdulshakuru Mohamed Ubuguyu, Issa Mohamed Mseketu maarufu kama Mtawa, Rajabu Thomas au Roja na Mohamed Ally Kadude maarufu kama Upolo.

Taarifa ya Sirro ilisema miili sita iliyobaki haikuweza kutambulika mara moja.

Taarifa pia iliwataja watuhumiwa wanaotafutwa kuwa ni Anafi Rashid Kapelo a.k.a Abuu Mariam, Hassan Haruna Kyakalewa a.k.a Abuu Salma Shujaa aka Dokta, Haji Ulatule, Shekhe Hassan Nasri Mzuzuri na Rashid Mtutula.

Kabla ya mafanikio hayo, bingo ya Sh. milioni 10 ilitangazwa na IGP Sirro kwa yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa wahusika wa mauaji hayo.

Kabla ya bingo ya IGP, Polisi mkoa wa Pwani ilikuwa imetangaza zawadi ya Sh. milioni tano kwa mwananchi yeyote ambaye atafanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa 12 ambao lilidai hujihusisha na mtandao wa mauaji hayo.

IGP Sirro alitangaza dau hilo la Sh. milioni 10 katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari Mei 31, jijini Dar es Salaam.

Alisema kwa yoyote atakayetoa taarifa sahihi ambazo zitawezesha kukamata wahusika wa mauaji ya kinyama dhidi ya raia na askari katika wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga mkoani Pwani, atapatiwa fedha hizo.

Source: Nipashe
IGP Sirro aeleza siri ya askari wake kuendelea kubaki Kibiti IGP Sirro aeleza siri ya askari wake kuendelea kubaki Kibiti Reviewed by Zero Degree on 12/11/2017 03:34:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.