Loading...

Maalim aagiza CUF walinde Ofisi kuu ya Zanzibar dhidi ya uvamizi

KATIBU Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amewataka wafuasi wa chama hicho kulinda ofisi kuu ya Zanzibar dhidi ya uvamizi unaotarajiwa kufanyika.

Akizungumza jana visiwani hapa, Maalim Seif alisema amepata taarifa kuwa Profesa Ibrahim Lipumba na kundi lake wanajiandaa kuvamia makao makuu ya chama hicho Zanzibar. 
Alitoa onyo kwa mtu yeyote ambaye atasogea kwenye makao makuu hayo kwa nia ya kufanya fujo, na kuwataka wanachama watiifu wa Zanzibar kuzilinda ofisi hizo.

Aidha, Maalim Seif alimshambulia mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Prof. Lipumba kwa kudai kuwavua madaraka wakurugenzi wa CUF Zanzibar na kuteua wakurugenzi wapya.

Akizungumza na wafuasi wake makao makuu ya CUF yaliopo Mtendeni, Maalim Seif alisema Prof. Lipumba hana mamlaka hayo kwani sio mwanachama tena wa chama hicho.
“Kitendo cha Lipumba kuwafukuza wakurugenzi wa CUF Zanzibar na kuwateua wengine, hana uwezo huo kwa sababu yeye si mwanachama," alisema Maalim Seif.

"Na hata angekuwa mwenyekiti halali, (bado) hana uwezo huo kwani wakurugenzi huthibitishwa na baraza kuu la taifa.”

“Vijana nawaambieni suala la kulinda ofisi hii ambayo ni makao makuu pamoja na ofisi ya wilaya iliyopo Kilimahewa Zanzibar sio kazi ya walinzi pekee," alisema Maalim Seif.

"Kila mwanachama azilinde ofisi ili Lipumba na watu wake wasisogee.”

Aidha, kiongozi huyo mkongwe kisiasa alimtaka Lipumba kutoshindana na yeye kwani hawalingani.

Alisema yeye amekuwa na mvuto mkubwa kwa wana CUF na ndiyo maana kila chaguzi amekuwa akipata kura nyingi tofauti na yeye.

Alisema Wazanzibar wana hamu ya serikali ya Zanzibar kuongozwa na CUF hivyo aliwataka wafuasi wa CUF kutowapa nafasi wasaliti wa chama hicho kukivuruga chama.

SALAM ZIMFIKIE

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad amemlaumu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja kwa kuandaa jeshi lake kupambana naye akiwa katika ziara za kichama katika mkoa huo.

“Salamu zimfikie Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja," alisema Maalim Seif. "Na aandae tu hayo mabomu na mimi ziara yangu nitafanya."

"Hakuna wa kunizuia wakati mimi ndiyo katibu mkuu wa CUF ambae nawatembelea wanachama wangu.”

Akizungumzia juu ya hilo, Kamanda Juma Sadi alimtaka Maalim Seif kupeleka ushahidi wa tuhuma alizotupa dhidi yake.

“Hayo maneno kapewa na nani? Na kama kapewa na wafuasi wake basi wanamdanganya, mimi sijaapa kusema maneno hayo aliyoyadai Maalim Seif dhidi yangu,”alisema Kamanda Sadi.

Kamanda huyo alifafanua kuwa mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa imepigwa marufuku Tanzania nzima, lakini vikao vya ndani hakuna katazo hilo ilimradi havivunji sheria za nchi.

Source: Nipashe
Maalim aagiza CUF walinde Ofisi kuu ya Zanzibar dhidi ya uvamizi Maalim aagiza CUF walinde Ofisi kuu ya Zanzibar dhidi ya uvamizi Reviewed by Zero Degree on 3/14/2017 12:50:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.